email us at
info@ntlp.go.tz
call us now

+255 (0) 26 2960150

TANZANIA YABORESHA VIWANGO VYA UTOKOMEZAJI UKOMA

TUTHAMINI HAKI NA UTU WA WAATHIRIKA WA UKOMA KWA KUTOKOMEZA UBAGUZI, UNYANYAPAA NA CHUKI

Serikali ya Tanzania imefikia viwango vya kidunia vya ubora utokomezaji ugonjwa wa Ukoma kuwa chini ya mgonjwa mmoja (1) kati ya watu elfu kumi (10,000) ambao ni sawa wagonjwa tisa (9) kati ya watu laki moja (100,000).

Hayo yamesema na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika maadhimisho ya siku ya Ukoma duniani ambapo yalifanyika katika makazi ya waathirika wa ugonjwa huo yaliyopo kijiji cha Msamalia kilichopo Hombolo mkoani Dodoma.

“Jitihada kubwa za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli zimeweza kupunguza viwango vya wagonjwa 43 kati ya watu milioni moja mwaka 2014 hadi kufikia wagonjwa 26 Kwa watu milioni moja Kwa mwaka 2019”. Alisema Waziri Ummy.

Aidha Mhe. Waziri Ummy Mwalimu alizitaja halmashauri 16 ambazo bado hazijafikia viwango hivyo.Halmashauri hizo ni pamoja na Manispaa ya Lindi, Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Masasi, Nanyumbu, Morogoro, Mvomero, Mpanda, Nkasi, Manispaa ya Shinyanga, Manispaa ya Kigoma, Kibaha, Mkinga na Tunduru.

Napenda kuchukua fursa hii kuzikumbusha Halmashauri hizi na mikoa kuongeza kasi ya kutokomeza Ukoma na kuhakikisha kaya zote hatarishi na zenye wagonjwa wa ukoma zinafikiwa, wanakaya wachunguzwe dhidi ya ugonjwa wa Ukoma na wale ambao tayari wanaugua wanatibiwa kikamilifu”. Alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy alisisitiza pia kwa kutoa wito kwa kila mwanajamii kujijengea tabia ya kujichunguza ngozi mwili mzima kila wakati na pale utakapoona dalili za ugonjwa wa Ukoma ambayo ni kuwa na baka au mabaka yenye rangi ya shaba mwilini basi nenda kituo chochote cha afya cha kutolea huduma kwa ajili ya uchunguzi zaidi na tiba kwani dawa za Ukoma zinatolewa bila malipo yoyote katika vituo vya kutolea huduma za afya. Kauli mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu siku ya Ukoma Duniani ni “TUTHAMINI HAKI NA UTU WA WAATHIRIKA WA UKOMA KWA KUTOKOMEZA UBAGUZI, UNYANYAPAA NA CHUKI”.

Mwisho Mhe. Waziri Ummy Mwalimu alitoa shukrani kwa watoa huduma za afya kote nchini kwa kazi nzuri wanazofanya katika kuhakikisha ugonjwa huu unatokomomezwa pamoja na kuwashukuru wanahabari kwa kuendelea kuhabarisha na kuelimisha jamii.Pia alichukua fursa hii kwa niaba ya serikali ya awamu ya tano kuyashukuru mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yanayounga mkono juhudi za serikali za kutokomeza ugonjwa wa Ukoma nchini kama vile Norvatis Foundation ya Uswisi, Germany Leprosy and Tuberculosis, Relief Association (GLRA) ya Ujerumani, Nippon Foundation chini ya Sasakwa Memorial Health Initiative ya Japan pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa michango yao ya hali na mali katika mapambano dhidi ya Ukoma.

 

 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsi Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akihutubia wananchi katika makazi ya waathirika wa ugonjwa wa Ukoma katika kijiji cha Msamalia kilichopo Hombolo mkoani Dodoma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiana na muathirika wa Ukoma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimvalisha viatu maalumu muathirika wa Ukoma kijijini hapo.