email us at
info@ntlp.go.tz
call us now

+255 (0) 26 2960150

TANZANIA YAFIKIA MALENGO YA MWAKA 2020 YA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI MAPYA YA KIFUA KIKUU

Tanzania inazidi kuendelea kupiga hatua katika kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa asilimia 18% kwa mwaka 2020 kwa mujibu wa ripoti ya shirika la afya Duniani (WHO).

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika kilele cha mkutano wa kupokea taarifa ya tathmini ya mpango mkakati wa tano wa mwaka (2015-2020) wa Kifua Kikuu na Ukoma februari 2020 uliofanyika mkoani Dodoma.

“Shirika la Afya Duniani (WHO) limekuja kufanya tathmini kwa kushirikiana na wataalamu wengine kutoka nje na ndani ikiwa ni kuona jinsi gani tumeyafikia malengo tuliojiwekea kwenye mpango mkakati wetu wa mwaka 2015 ikiwemo kuongeza kasi ya kuwafikia wagonjwa kwa asilimia 29 zaidi” alisema Dkt. Chaula.

Kifua Kikuu kinaenezwa kwa njia ya hewa hivyo amewataka wananchi kuepuka msongamano wa watu wengi, kuboresha usafi wa mazingira, kuishi kwenye nyumba zenye hewa safi na salama na amewataka wananchi pindi wanapoona dalili za kifua kikuu kama kupungua uzito, kutokwa na jasho jingi nyakati za usiku, kukohoa kwa muda wa wiki mbili mfululizo basi wafike kituo cha afya kwa uchunguzi zaidi juu ya afya zao na kupatiwa matibabu na endapo watabainika kuwa na kifua kikuu wataanzishiwa matibabu kwani matibabu ni bure bila malipo na yanatolewa kuanzia ngazi ya Zahanati.

Aidha Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Dkt. Zuweina Kondo-Sushy aliwashukuru wote waliofanikisha kukamilika kwa zoezi hilo la tathmini na kujivunia mafanikio makubwa ya mpango kwa kuongeza uwezo wa ugunduzi na kuibua wagonjwa wengi zaidi kutoka asilimia 29% mwaka 2015 hadi asilimia 53% mpaka sasa. Tanzania ni miongoni mwa nchi saba Duniani kufikia malengo hayo ya mwaka 2020 ya kupunguza maambukizi mapya

“Kwa mwaka jana tuu tumeweza kugundua wagonjwa karibia 82140, kadri unavyogundua wagonjwa wengi ndivyo utakavyo stopisha maambukizi”. Alisema Dkt. Zuweina.

Dkt. Zuweina pia amesema kwa upande wa watoto mpango umeweza kufikia lengo la kidunia kwa kuwaibua watoto wengi kwa kiasi cha asilimia 15% ambapo idadi hii ni idadi ya juu iliyotajwa na Shirila la Afya Duniani (WHO) kwa nchi ambazo zina matatizo makubwa  ya kifua kikuu ambapo.

Kwa upande wa mafanikio ya Ukoma mpango umefanikiwa kupunguza maambukizi mapya na hadi sasa ni halmashauri 16 tu ndio zenye viwango vikubwa vya ugonjwa huu. Mafanikio haya makubwa yametokana na juhudi za serikali hii ya awamu ya tano chini ya Mhe. Raisi John Pombe Magufuli.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula akiongea na wataalamu wa ndani na nje ya nchi (hawapo pichani) wakati wa kupokea taarifa ya tathmini  ya mapitio ya mpango mkakati wa tano (2015-2020) wa Kifua Kikuu na Ukoma.

Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Dkt. Zuweina Kondo akiongea na waandishi wa habari wakati uwasilishwaji wa taarifa ya tathmini ya mpango mkakati wa tano (2015-2020) wa Kifua Kikuu na Ukoma.

Mtaalamu kutoka nje ya nchi Dkt. Wilfried Nkhoma akipokea cheti cha kuthaminiwa kutoka kwa Dkt. Zainab Chaula wakati wa kilele cha mkutano uwasilishwaji wa taarifa ya tathmini ya mpango mkakati (2015-2020) wa Kifua Kikuu na Ukoma.

Wataalamu wa ndani na nje ya nchi wakiwa katika mkutano wa uwasilishwaji wa taarifa ya tathmini ya mpango mkakati  wa tano (2015-2020) wa kifua Kikuu na Ukoma.