email us at
info@ntlp.go.tz
call us now

+255 (0) 26 2960150

VIONGOZI WA DINI WASAINI MAAZIMIO YA MAPAMBANO DHIDI YA KIFUA KIKUU NCHINI

Na. WAMJW

Serikali ya Tanzania inatenga mabilioni mengi katika kushughulikia masuala ya afya nchini hususani kwenye upande wa tiba ambapo gharama za matibabu zinakuwa kubwa sana.

Hayo yamesemwa na Spika wa Bunge la Jamhuri Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai wakati wa kusaini tamko la maazimio ya viongozi wa dini lililobeba ajenda ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua kikuu (TB) nchini jijini hapa.

‘Wananchi wanadhani kuwa Wizara ya Afya inasimamia tu tiba, hapana tusisahau kinga ni muhimu sana dhidi ya magonjwa nchini,tutakaposimamia kinga serikali itakuwa inaokoa gharama kubwa kwenye matibabu na pia kupunguza mzigo mkubwa wa kugharamia matibabu kama nchi’ Alisisitiza Mhe. Ndugai

Aidha, amewashukuru viongozi hao wa dini kwa ahadi pamoja na kusaini azimio la kusimamia na kusemea kwa waumini wao suala la TB hivyo anayo Imani watalibeba na kulitekeleza na kuwafanya wananchi wengi kupata uelewa juu ya ugonjwa huo na kujitokeza mapema kwenda kupima afya zao na hvyo kuanza dawa na kutoambukiza watu wengine.

Awali akiongea na viongozi hao Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Wizara yake inaendelea kubuni mikakati ya kutokomeza TB inchini kama mikakati Madhubuti yaliyowekwa kwa mara ya kwanza na baraza kuu la umoja wa mataifa lililokutana septemba mwaka 2018 na kuweka maazimio ya kuongeza kasi ya kutokomeza TB ifikapo mwaka 2030.

Maambukizi mapya ya TB nchini yamepungua kwa asilimia 18 kulinganisha na hali ya mwaka 2015 na hivyo kufanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi saba Duniani ambazo zipo katika mwelekeo sahihi wa kufikia malengo ya mpango mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kutokomeza TB kwa hatua ya kwanza ya mwaka 2020.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa vifo vitokananyo na TB peke yake vimepungua kutoka 30,000 mwaka 2015 hadi 22,000 mwaka 2018 na hii ni sawa na punguzo la asilimia 27, “Licha ya mafanikio,nchi bado ina vifo vingi vinavyosababishwa na TB ambapo kwa sasa takribani watu sitini hufariki kila siku hapa nchini” , alisema.

Hata hivyo Waziri huyo wa Afya amesema kuwa hadi kufikia mwaka huu serikali ina vituo 103 vinavyotoa huduma za wagonjwa wenye kifua kikuu sugu ukilinganisha na kimoja mwaka 2015 pamoja na uboreshaji wa mifumo ya uchunguzi na ugunduzi wa TB kwenye vituo vya huduma za afya, upanuzi wa matumizi ya hadubini za kisasa za LED na kuongezeka kwa mashine za kisasa zinazopima vimelea vya TB kwa njia ya vina saba za GenXpert zipatazo 238 ambazo kwa sasa zinapatikana kwenye mikoa yote nchini.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai akiongea na viongozi wa dini (hawapo pichani)  wakati wa mkutano wa viongozi wa dini wa Taifa na wa Kanda ya ziwa ambapo viongozi wa di I waliitia Saini maazimio ya kupambana dhidi ya Kifua kikuu jijini Mwanza.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimua, akiongea jamno wakati wa mkutano wa viongozi wa dini ambapo alisema wanayo Imani na viongozi wa dini kwani wanawafikia wananchi wengi.

Mkuu wa mkoa Mwanza Mhe. John Mongella akiwakaribisha viongozi mbali mbaliwa Serikali wakitaifa, Viongozi wa dini na viongozi wa Taasisi zisizo za kiserikali na wageni wengine katika mkoa wa Mwanza.

Baadhi ya viongozi wa dini wakifuatilia mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza.

Viongozi wa dini wakisaini maazimio ya kushiriki mapambano ya kutokomeza kifua kikuu wakishuhudiwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Job Ndugai, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na viongozi wengine wa kiserikali