Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia wa kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund ATM), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la STOP TB Partnership inatarajia kufanya mkutano wa Kikanda ya Afrika wa masuala ya Kifua Kikuu jijini Arusha kuanzia tarehe 04 hadi 07 Julai 2023 katika hoteli ya Mount Meru. Mkutano huu utashirikisha washiriki zaidi ya 70 kutoka jumla ya nchi 21 Barani Afrika na nje ya Afrika.
Washiriki wa mkutano huu muhimu wanatarajiwa kuwa Makatibu Wakuu wa Wizara ya Afya na Mameneja Mpango wa Programu za Kifua Kikuu kutoka nchi 15 barani Afrika. Mkutano huu una malengo ya kupata uzoefu wa Makatibu Wakuu katika kuchochea kasi ya kutafuta rasimali na utashi wa kisiasa katika kupambana na Kifua Kikuu Barani Afrika, kubaini changamoto na vikwazo vinavyochelewesha kufikia malengo ya kutokomeza Kifua Kikuu Duniani ifikapo 2030, kubadilishana uzoefu wa afua bora za Kifua Kikuu (TB best practices) miongoni mwa nchi za Afrika pamoja na maandalizi ya Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kifua Kikuu (UN High Level Meeting).
Katika Mkutano huu washiriki watapa fursa ya kutembelea vituo vya afya na asasi za kijamii zinazoshughulika na Kifua Kikuu katika Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Vilevile kuona mnyororo wa huduma za Kifua Kikuu zinavyotolewa kutoka ngazi ya jamii hadi Kituo cha Afya. Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa mkutano huo