Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amefungua Kampeni harakishi ya ubuaji wa wagonjwa wa Kifua Kikuu kwa Mkoa wa Shinyanga na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kupima na kupatiwa dawa bure pasipo kuwa na gharama yoyote katika hilo.
RC macha ameyasema hayo tarehe 8 Februari, 2025 katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni na watalaam wake, Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Masumbuko, viongozi wa Vyama vya siasa, Kamati ya Amani Mkoa na wananchi.
"Baada ya ufunguzi huu, nitoe wito sasa kwa wananchi wetu kujitokeza kuja kupima na kwa wale watakaobainika kuwa na ugonjwa wa TB watapatiwa dawa bila malipo yoyote, lengo la Serikali ni kuona wananchi wake wanakuwa na afya ili wazalishe mali na kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla," amesema RC Macha.
Amesema kuwa kwa Mkoa wa Shinyanga watu wenye ugonjwa wa kifua kikuu ni takribani 2,903 ambapo watu 1,349 wanatjwa kuwa bado hawajafikiwa ambao ndio wanatafutwa kupitia kampeni hii, huku akisisitiza kuwa ugonjwa huu ni hatari sana na una ambukizwa kwa njia ya hewa.
Katika hotuba yake RC Macha amesisitiza kwamba, mgonjwa mmoja mwenye Kifua Kikuu kwa mwaka mmoja anaweza kuambukiza watu 20 na kwamba hatua zisipochukuliwa mapema tatizo laweza kuwa kubwa, na sababu Serikali iinayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuja na kampeni hiyo ili kuokoa maisha ya wananchi.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, CP. Hamduni alisema kuwa baada ya ufunguzi huo utekelezaji unakwenda kufanyika katika Halmashauri zote 6 zinazounda Mkoa huku akisisitiza utekelezajj uendane na kichwa cha habari kama kinavyosena kuwa ni harakishi kwa wagonjwa wa kifua kikuu ili kuweza kuokoa maisha yao na kuweka kinga kwa wale ambao hawajaambuiizwa.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Daktari. Luzila John alisesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mwaka 2023 pekee watu takribani Milioni 10.8 waligundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu, na ambapo zaidi ya Milioni 2 walifariki dunia.