Phone: +255 (0) 26 2960150 | Email: info@ntlp.go.tz
Home / Media / Blog / WIZARA KUENDELEA KUSIMAMIA UTOAJI WA HUDUMA ZA KIFUA KIKUU NA UKOMA SANJARI NA MPANGO MKAKATI WA SITA (2020/21 - 2025/26) WA MAPAMBANO DHIDI YA KIFUA KIKUU NA UKOMA.

WIZARA KUENDELEA KUSIMAMIA UTOAJI WA HUDUMA ZA KIFUA KIKUU NA UKOMA SANJARI NA MPANGO MKAKATI WA SITA (2020/21 - 2025/26) WA MAPAMBANO DHIDI YA KIFUA KIKUU NA UKOMA.

image

Bungeni, Dodoma.

Wizara ya Afya itaendelea kusimamia utoaji wa huduma za Kifua Kikuu na Ukoma kwa mujibu wa Mpango Mkakati wa Sita (2020/21 - 2025/26) wa kupambana na magonjwa haya. Hayo yamesemwa tarehe 13 Mei, 2024 na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Katika jitihada za kupambana na magonjwa ya kuambukiza, yasiyoambukiza, mlipuko na kutoa huduma za dharura nchini, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 84.864 ili kufanikisha mpango huu, ikiwemo ununuzi wa vifaa tiba, vitendanishi na dawa za kutibu Kifua Kikuu na Ukoma.

Mhe. Ummy alieleza kuwa malengo makuu ya mpango huu ni kupunguza maambukizi mapya ya Kifua Kikuu kwa asilimia 50, kupunguza vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu kwa asilimia 75 na kutokomeza Ukoma katika Halmashauri zenye wagonjwa wa Ukoma ifikapo mwaka 2025. Hadi kufikia Machi 2024, Tanzania imefanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya Kifua Kikuu kwa asilimia 36, kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mwaka 2015 hadi wagonjwa 195 kwa kila watu 100,000 mwaka 2023.

Aidha, takwimu zinaonyesha vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu vimepungua kwa asilimia 67 kutoka vifo 56,000 mwaka 2015 hadi vifo 18,000 mwaka 2023 na hivyo kuwa kwenye njia sahihi ya kufikia lengo la kupunguza maambukizi kwa asilimia 50 na vifo kwa asilimia 75 pindi ifikapo mwaka 2025. Mafanikio haya yametokana na kuwashirikisha watoa huduma za afya ngazi ya jamii hasa wale waliougua kifua kikuu na kupona, waganga wa Tiba Asili na sekta binafsi.

Aidha, takwimu zinaonyesha kuwa vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu vimepungua kwa asilimia 67, kutoka vifo 56,000 mwaka 2015 hadi vifo 18,000 mwaka 2023. Hivyo, nchi ipo kwenye njia sahihi ya kufikia lengo la kupunguza maambukizi kwa asilimia 50 na vifo kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2025. Mafanikio haya yamechangiwa na ushirikiano na watoa huduma za afya ngazi ya jamii hasa wale waliougua kifua kikuu na kupona, waganga wa tiba asili na sekta binafsi.

Vilevile, katika kipindi hiki jumla ya wagonjwa 194 wa Kifua Kikuu Sugu waligundulika na kuanzishiwa matibabu ambao ni sawa na asilimia 43 ya lengo la kugundua wagonjwa 453 ikilinganishwa na wagonjwa 266 waliogundulika katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23 sawa na asilimia 40 ya lengo la kuibua wagonjwa 664 wa Kifua Kikuu Sugu.

Sambamba na hayo, Mhe. Ummy aliendelea kwa kusema katika kuimarisha huduma za upimaji wa Kifua Kikuu, Serikali kupitia Wizara ya Afya imenunua mashine za upimaji za GeneXpert 75 na Truenat 110 ambazo zitasimikwa kwenye vituo 110 vya kutolea huduma za afya vya ngazi ya msingi na Hospitali mpya za Halmashauri 70 ambazo zitafanya jumla ya GeneXpert na Truenat kufikia 411 na 152 mtawalia. Wizara imeendelea kutoa huduma mkoba za kliniki tembezi zenye uwezo wa kutoa huduma za uchunguzi na ugunduzi kwa magonjwa ya Kifua Kikuu na magonjwa mengine ya mfumo wa njia ya hewa katika maeneo yenye makundi hatarishi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Aidha, Wizara itaendelea kuimarisha huduma za utoaji wa elimu juu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa jamii kupitia redio za kijamii, mitandao ya kijamii, runinga na machapisho.

Pia, Waziri Ummy alieleza kuwa katika jitihada za kutokomeza Ukoma nchini, Wizara imeendelea kusimamia huduma za uchunguzi na tiba kwa wale wanaogunduliwa kuwa na Ukoma. Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, jumla ya wagonjwa 761 waligundulika na Ukoma, ikilinganishwa na wagonjwa 1,227 waliogundulika katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23. Sambamba na uibuaji huo, wanakaya 847 walifanyiwa uchunguzi na wagonjwa 28 walibainika na kuanzishiwa matibabu. Wizara pia imeendelea kutoa vifaa tiba saidizi kwa kugawa jozi 240 za viatu maalum ili kupunguza athari za ulemavu kwa waathirika wa Ukoma.

Mwisho