Phone: +255 (0) 26 2960150 | Email: info@ntlp.go.tz
Home / Media / Blog / WIZARA YA AFYA ,OR-TAMISEMI, CIHEB TANZANIA NA WADAU WASHIRIKIANA KATIKA KAMPENI YA KUIBUA WAGONJWA WA TB MANISPA YA TEMEKE

WIZARA YA AFYA ,OR-TAMISEMI, CIHEB TANZANIA NA WADAU WASHIRIKIANA KATIKA KAMPENI YA KUIBUA WAGONJWA WA TB MANISPA YA TEMEKE

image

Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Shirika lisilo la Kiserikali la “CIHEB Tanzania” kwa kushirikia na wadau tarehe 14 Juni, 2025 iliendesha kampeni maalum ya siku tatu ya kuwatafuta na kuwaibua wagonjwa wa Kifua Kikuu na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa kwa wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na maeneo jirani. 

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Ayubu Kibao,  amelishukuru shirika hilo kwa kushirikiana vizuri na Serikali katika kuwahudumia wananchi kwa kusogeza huduma katika ngazi ya jamii ambapo ndipo wagonjwa wengi zaidi hupatikana.

“Kampeni hii itatusaidia kuwaibua wagonjwa wengi zaidi ambao wapo katika jamii na kuwaweka kwenye matibabu na kupelekea kuzuia kasi ya maambukizi mapya katika jamii hasa Wilaya ya Temeke na maeneo jirani” alisema Dkt. Kibao.

Aidha, Dkt. Wanze Kohi Mtaalam Mshauri wa Kifua Kikuu kutoka Shirika la CIHEB Tanzania alisema wameamua kufanyia kampeni hii katika kata ya Chamazi kwa sababu ya eneo hilo kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi ya ugonjwa  wa TB.

“Kampeni hii imelenga kuifikia jamii yote ya wakazi wa Temeke na maeno jirani, tumedhamiria kuwachunguza, kutoa elimu na hamasa kuhusu ugonjwa wa TB na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa kwa watu 1500 na zaidi” alisema Dkt. Wanze

Nae Bw. Bakari Athumani Milazi Afisa Mtendaji Kata ya Chamanzi amesema wanashirikiana bega kwa beka na wadau mbalimbali waliopo katika kata hiyo kwa kuwapelekea huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ikiwemo Kifua Kikuu.

“Katika kata hii tunatumia mbinu mbali mbali za kuhamasisha na kuelimisha wana jamii kuhusu ugonjwa wa TB kwa kuwa na ratiba maalum ya kutembelea kaya kwa kaya kwa kuwatumia watoa huduma za afya ngazi ya jamii, matamasha ya burudani pamoja na michezo” alisema Bw. Bakari.

Aidha, Mwenyekiti wa Asasi ya Kiraia ya masuala ya Kifua Kifuu MKIKUTE, Bw. Gabriel Majaliwa alisema katika kampeni hiyo wamejipanga kushirikiana na Serikali na wadau kuingia katika masoko, maskani wanaotumia dawa za kulevya, nyumba kwa nyumba na vijiwe vya bodaboda kwa kuwatangazia wananchi huduma zinazotolewa katika eneo hilo kwa kutumia gari maalumu la Kliniki tembezi ambapo wananchi wanachunguzwa afya zao na wanapobaika kuwa na ugonjwa wa TB wanaanzishiswa matibabu.

Huduma hizo za uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu zinatolewa bure bila gharama yoyote.

images.jpg