Dhana potofu katika jamii ya kuwa kila mtu anayeugua ugonjwa wa Kifua Kikuu huwa ana maambukizi ya VVU imekuwa chanzo cha unyanyapaa katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Huduma za Matunzo na Kinga Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Dkt. Allan Tarimo mapema wiki hii alipokuwa katika Mkutano wa 31 wa kisayansi wa tafiti ya afya za binadamu uliofanyika katika ukumbi wa mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Si kila mtu mwenye kifua kikuu ana maambukizi ya VVU maana kumekuwa na unyanyapa katika jamii kwamba kila mwenye kifua kikuu ana maambukizi ya VVU si kweli”
Aliongeza kwa kusema ugonjwa wa Kifua Kikuu hauenezwi kwa kurogwa, kurithi, kula na mgonjwa au kushirikiana vyombo vya chakula na mgonjwa bali huenezwa kwa njia ya hewa pale mgonjwa ambaye hajaanza matibabu anapo kohoa au kupiga chafya. Aidha,mgonjwa ambae amekwisha anza matibabu ana uwezekano mdogo sana wa kuambukiza TB.
Mikakati iliyopo kwa sasa katika kupunguza unyanyapaa kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu ni pamoja na kuongeza uelewa na uhamasishaji kwa jamii ambapo kumekuwa na jitihada za makusudi za kutoa elimu katka jamii.
Dkt Tarimo ametoa rai kwa jamii pindi waonapo dalili za Kifua Kikuu kama kukohoa zaidi ya wiki mbili au zaidi, kupungua uzito, homa za mara kwa mara hasa nyakati za jioni, kutokwa na jasho jingi kuliko kawaida hasa nyakati za usiku, hivyo kujitokeza katika vituo vya afya kwa uchunguzi zaidi kwani huduma za uchunguzi na matibabu ya Kifua Kikuu hutolewa bila malipo kwa vituo vya afya vya umma na binafsi.
Mratibu wa Huduma za Matunzo na Kinga kutoka Mpango wa Taifa wa Kifua Kiku na Ukoma Dkt. Allan Tarimo
Mratibu wa Huduma za Matunzo na Kinga kutoka Mpango wa Taifa wa Kifua Kiku na Ukoma Dkt. Allan Tarimo (Kulia) akimuelezea Mkuu wa Kitengo cha Maboresho katika sekta ya Afya Dkt. Catherine Joachim namna mashine ya GeneXpert na Hadubini zinavyotumika katika ugunduzi na uibuaji wa Kifua Kikuu.
Wageni waalikwa wakifuatilia mawasilisho juu ya tafiti mbalimbali kuhusu afya ya binadamu katika mkutano wa 31 wa kisayansi wa tafiti za afya za binadamu uliofanyika katika ukumbi wa Mwl. Julius K. Nyerere jijini Dar es Salaam.