Nchi wanachama wa jumuiya ya SADC zimekutana kujadili mikakati mbalimbali ya kutokomeza Kifua Kikuu katika umoja huo. Kikao hicho kimefanyika jijini Lusaka nchini Zambia kuanzia tarehe 24 mpaka 28 Juni. Jumla ya nchi 14 za jumuiya hiyo zimeshiriki mkutano huo. Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kupokea na kupitisha taarifa za mwaka za utekelezaji sambamba na kubadilishana uzoefu kwa nchi wanachama ambazo zimepambana na ugonjwa wa TB.
Wadau mbalimbali kutoka nchi wanachama wa SADC wameweza kupitia na kuidhinisha taarifa za mwaka za mapambano ya Kifua Kikuu za mwaka 2023 pamoja na kupitia takwimu na viashiria vyote muhimu vitakavyowezesha kutokomeza Kifua Kikuu pindi ifikapo mwaka 2030. Taarifa hizi ni muhimu na zitasaidia kuandaa mikakati mipya na kutafuta rasilimali zitakazowezesha kupambana na Kifua Kikuu katika nchi za jumuiya hiyo na kufikia malengo ya kidunia ya kutokomeza ugonjwa huo pindi ifikapo mwaka 2030. katika mkutano mwingine wa kutokomeza Kifua Kikuu migodini kupitia mradi wa kikanda wa Kifua Kikuu maeneo ya migodini - (SADC TB in the mining sector Phase III) uliofanyika kando ya mkutano huo ulijadili taarifa mbalimbali za utekelezaji kupambana na TB zilizofanyika katika maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo. Taarifa hizi zilikusanywa kutoka nchi mbalimbali zilizopo katika ukanda huo wa SADC na kujadiliwa kwa kina sambambana na takwimu zilizopatikana juu ya athari zilizotokana na uchimbaji wa madini ambazo zimeathiri wachimbaji wadogo wadogo. Aidha, katika mkutano huo umeweza kupitia na kuthibitisha taarifa za kitafiti za wachimbaji wadogo wadogo zilizokusanywa na mtaalamu muelekezi aliyefanya tafiti katika nchi za ukanda huo zipatazo 8 ikiwemo Tanzania zinazopambana na Kifua Kikuu maeneo ya migodini. Matokeo ya utafiti huu yatasaidia kujua idadi ya wachimbaji wadogo wadogo, namna mgawanyiko wao ulivyo, kujua upatikanaji wa huduma za afya katika maeneo yao pamoja na chagamoto zinazowakibili za kiafya. Katika hatua nyingine, SADC imeunda kamati maalum ya kusimamia miongoni mwa nchi wanachama kutokomeza Kifua Kikuuu ifikapo 2030. Kamati hii ambayo Tanzania inauwakilishi inachukua jukumu la kutekeleza dira mkakati ya SADC End TB 2030 Mwisho wa mikutano hii, inategemewa kuwepo na maazimio yatakayokuwa na mikakati madhubuti ya kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu na changamoto zingine za kiafya zinazowakabili wachimbaji wadogo wadogo katika maeneo ya migodi katika nchi za ukanda wa SADC.
Maazimio hayo yatasambazwa katika nchi wanachama kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wake. Jumla ya nchi 14 kutoka katika jumuiya hiyo zimeshiriki, kwa upande wa Tanzania ujumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi ajira na Ulemavu kupitia OSHA, Wizara ya Afya kupitia NTLP, Wizara ya Madini pamoja na washiriki mbalimbali kutoka katika vyama vya wachimbaji wadogo wadogo nchini wameshiriki katika mikutano hiyo muhimu. Mwisho