Phone: +255 (0) 26 2960150 | Email: info@ntlp.go.tz
Home / Media / Blog / Tanzania yaunga mkono jitihada za Shirika la Afya Duniani na Mashirika ya Kitaifa kupambana na Magonjwa

Tanzania yaunga mkono jitihada za Shirika la Afya Duniani na Mashirika ya Kitaifa kupambana na Magonjwa

image

TANZANIA YAUNGA MKONO JITIHADA ZA SHIRIKA LA AFYA DUNIANI NA MASHIRIKA YA KIMATAIFA KATIKA KUPAMBANA NA MAGONJWA

Na.WAF-Geneva

Serikali ya Tanzania inaunga mkono jitihada za Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na mashirika mengine ya Kimataifa katika kupambana na magonjwa.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwenye mkutano wa 75l wa Shirika la Afya Dunia unaoendelea jijini Geneva, Uswisi. 

Waziri Ummy ambaye ameongoza ujumbe huo amewasilisha  kauli ya Tanzania ambapo amelipongeza Shirika hilo kwa kutoa ushirikiano kwa wanachama wake na kuunga mkono kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Health for Peace, Peace for Health” yaani “Dumisha Amani, Linda Afya” 

Waziri Ummy amefafanua kwamba kauli mbiu hiyo ni muhimu katika kutambua kuwa, pasipo na amani, utoaji wa huduma za afya mara nyingi huwa hatarini.

"Tanzania inatambua madhara makubwa ya kiuchumi na kijamii yaliyotokana na UVIKO-19, na pia athari zake kwenye mifumo ya afya na maisha ya watu kwa ujumla.Tumeshuhudia mawimbi kadhaa ya mlipuko wa ugonjwa huo na tunatambua kazi kubwa iliyofanywa na Shirika la Afya Duniani katika kuratibu mapambano dhidi ya mlipuko huu, na kuimarisha juhudi za kuboresha utayari wa kukabiliana na dharura na majanga".Amesema Waziri Ummy

Hata hivyo amesema kuwa jitihada za pamoja zinahitajika ili kuimarisha uwezo wa sekta ya afya katika utayari wa kukabiliana na dharura na majanga kwa uratibu madhubuti, huku ukizingatia kuwa na mifumo ya afya iliyo thabiti pamoja na mazingira yenye amani. 

Alieleza kuwa Tanzania imejidhatiti katika kuimarisha usalama wa afya katika mwelekeo wa kuhakikisha inafika lengo la Afya kwa Wote.

Aidha, Waziri Ummy alikumbushia kuwa pamoja na nchi kutoa kipaumbele katika kushughulikia janga la UVIKO-19, ni vema nchi zikaendelea na jitihada za kutatua changamoto ya uhaba mkubwa wa watumishi wa Afya.

"Kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza,kasi ndogo ya kupunguza magonjwa ya kuambukiza kama vile UKIMWI na Kifua Kikuu, masula ya Lishe,  Polio, Huduma za Chanjo, pamoja na afya ya akina mama na watoto, tuna imani kuwa mkutano huu utakuwa na mafanikio kwa wote na tunaunga mkono ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi wa WHO".Aliongeza