Phone: +255 (0) 26 2960150 | Email: info@ntlp.go.tz
Home / Media / Blog / WADAU WA MAPAMBANO YA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU NA UKOMA WAKUTANA KUFANYA MAPITIO YA HALI YA MAGONJWA HAYO NCHINI

WADAU WA MAPAMBANO YA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU NA UKOMA WAKUTANA KUFANYA MAPITIO YA HALI YA MAGONJWA HAYO NCHINI

image

Mpango wa Taifa wa Kifua kikuu na Ukoma kwa kushirikiana na wadau wamefanya kikao kazi kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwenendo wa mapambano ya kutokomeza Kifua Kikuu na Ukoma nchini. Kikao hicho kimefanya agosti 21, 2024 jijini Arusha.

Akifungua kikao cha mapitio ya takwimu za Kifua kikuu na ukoma  Mkuu wa Programu kutoka Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim amesema Tanzania imepiga hatua katika kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini kwa kuweza kupunguza maambukizi mapya ya Kifua Kikuu kwa asilimia 40 na vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu kwa asilimia 67 kufikia mwaka 2023.

Dkt. Catherine alibainisha kuwa pamoja na mafanikio makubwa ambayo Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma kwa kushirikiana na wadau wameyapata, bado kuna maeneo ambayo yana changamoto na yanahitaji mikakati jumuishi katika utatuzi wake, alibainisha maeneo hayo ni pamoja na elimu na hamasa juu ya  uelewa wa magonjwa haya kwa jamii.

“Endeleeni kuimarisha ushirikiano katika kuendelea kupaza sauti za uelewa wa Kifua Kikuu na Ukoma katika ngazi zote za utoaji wa huduma kuanzia kwenye jamii hadi kwa watumishi huku tukitumia uratibu wa Mpango Jumusihi wa Uwajibikaji wa kisekta MAF-TB” alisema Dkt. Catherine. 

Aidha Dkt. Catherine aliitaka Programu ya TB na Ukoma pamoja na watekelezaji wote wa mkakati wa Kifua Kikuu na Ukoma nchini kuhakikisha wanaboresha uibuaji wa wagonjwa wa Kifua Kikuu, Kifua Kikuu Sugu na Kifua Kikuu kwa makundi maalum kwa kuweka nguvu katika maeneo yanayohisiwa kuwa na wahisiwa wa TB wengi hasa kwa Watoto, Wachimbaji wadogo wadogo wa migodi na makundi mengine ili kufikia malengo ya dunia ya kutokomeza magonjwa haya pindi ifikapo mwaka 2030 na 2035.

images-1.jpg

Katika hatua nyingine, Meneja Mpango wa Kifua Kikuu na Ukoma Dkt.Riziki Kisonga amesema kuwa kikao kazi hiki kinatarajia kutoa ushauri na mapendekezo bunifu yatakayo toa mwelekeo chanya katika kuelekea kufikia malengo ya kutokomeza magonjwa haya nchini ifikapo mwaka 2030. 

Mwisho.