Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau wa Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA - HC) wameendesha mafunzo kwa Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya Serikali na binafsi kutoka nchi 12 juu ya kuandika habari sahihi kuhusu ugonjwa wa Kifua Kikuu hasa katika maeneo ya migodi.
Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyikaj jijini Dar es Salaam, Afisa Mawasiliano wa Mradi wa ECSA - HC, Bw. Justine Mahimbo amesema mafunzo hayo yamewakutanisha Wanahabari 36 kutoka katika nchi 12 za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) ambazo ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Namibia, Zambia, Malawi, Zimbabwe, Msumbiji na wenyeji Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Bw. Mahimbo amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo Wanahabari kuhusu uelewa wa ugonjwa wa kifua Kikuu katika namna ya uambukizaji, matibabu na jinsi ya kuzia kuenea kwa ugonjwa huo katika jamii hasa maeneo ya migodi.
"Lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha Wanahabari wanakuwa na uelewa wakutosha wa namna Kifua Kikuu kinavyo ambukizwa, njia za kueneza, kujikinga pamoja na kuweza kutoa elimu na uhamasishaji kwa jamii katika kutokomeza ugonjwa huo."
Aidha, Mratibu wa Mawasiliano na Uhamasishaji Jamii wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Tanzania, Bw. Julius Mtemahanji amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kupambana na Ugonjwa wa Kifua Kikuu hasa katika maeneo ya migodi hapa nchini.
"Wanahabari wana jukumu kubwa katika kuelimisha na kuhamasisha jamii dhidi ya mapambano ya Kifua Kikuu hivyo mafunzo haya yanawajengea uwezo wa kuandika habari zenye weledi na sahihi juu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu."
Vile vile Bw. Mtemahanji ameushukuru uongozi wa ECSA - HC kwa kuchagua Tanzania kuendesha mafunzo hayo kwani yataongeza chachu katika kuandika habari za mapambano dhidi ya Kifua Kikuu hapa nchini.
MWISHO.