Wasimamizi wa mradi wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria “Global Fund” kutoka makao makuu ya GLobal Fund Geneva, Uswisi wamekutana na watekelezaji na wadau wa mradi huo nchini.
Lengo la kikao kazi hicho ni kujadili utekelezaji wa mipango kazi ya mradi huo nchini kupitia mtekelezaji mwenza wa Jimbo la Serikali (PR1), aidha kupokea taarifa kutoka “Global Fund” kuhusu matokeo ya utekelezaji wa kazi zilizotekelezwa kwenye mzunguko wa 6 (Global Fund Cycle 6) wa mwaka 2021-2023 na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi kupitia fedha za Mfuko wa dunia kwenye mzunguko wa 7 kwa kipindi cha mwezi Januari mpaka Agosti, 2024.
Akifungua kikao hicho Mgeni rasmi Bw. Lusajo Ndagire kwa niaba ya Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya aliwashukuru Mfuko wa Dunia kwa Kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
“Tangu mwaka 2002, Mfuko wa Dunia umekwisha wekeza dola za kimarekani bilioni 3.8 nchini Tanzania kwa ajili ya kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria, kuimarisha mifumo na kuchochea kupunguza maambukizi ya magonjwa haya pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya” alisema
Bw. Lusajo pia alisema kikao hicho kitatumika kama jukwaa muhimu la kujadili mafanikio na kuweka mikakati ya pamoja katika kushughulikia changamoto zilizopo ili kuwezesha kufikia mafanikio na malengo ya kutokomeza magonjwa hayo nchini pindi itakapofikia mwaka 2030.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wataalamu mbalimbali wanaotekeleza miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Dunia “Global Fund” kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Afya,OR TAMISEMII ,TACAIDS, na wadau mbalimbali wakiwepo Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na PEPFAR. kikao kazi hicho kinatarijiwa kuhitimishwa siku ya Alhamis tarehe 12 Septemba 2024.